Filamu ya Simu ya Kifo imeitangaza Tabora Ulimwenguni


Filamu ya Simu ya kifo ya Tripod Media yakamilika: Muongozaji wake Hammie Rajab ahofia nakala za filamu hiyo hazitatosha.
¬¬¬¬¬¬¬¬¬¬¬¬¬¬¬¬ ________________________________________________________

Kama unafikiri umekwisha iona filamu bora ya kiswahili ya upelelezi … bado hujaiona Simu ya kifo.. ndivyo anavyoeleza Muongozaji wa Filamu hiyo Hammie Rajab. Imechezwa Tabora mtaa wa Rufita na kuwakumbusha watu wazima enzi zao za shule waliposoma hadithi yake, zaidi ya miaka 30 iliyopita. IGP alitoa baraka majengo ya Polisi Tabora yatumike, RPC Tabora asema “..niliisoma shule…” askari wake hawakujua wakampigia saluti Inspekta Wingo.! Wakati inatayarishwa.

Katika makala hii Mwandishi wetu ameongea na Muongozaji wa filamu hiyo Hammie Rajab ambaye licha ya ugwiji wake wa kutunga na kuongoza sinema nyingi amekiri kuwa mtunzi wa hadithi hiyo Faraji Katalambulla ni kiboko, akasema angekuwa na nguvu angembeba juu kwa juu kuonyesha furaha yake.Fuatana na mwandishi wetu katika simulizi za filamu hii ya dakika 120.
_____________________________________________________________________

Dakika 120 za filamu hii zinaisha kama sekunde !

Ni filamu ya dakika 120 inayotokana na simulizi za kitabu cha Faraji Hussein Hassan Katalambula kiitwacho Simu ya Kifo alichokiandika miaka ya 1960. Baada ya zaidi ya miaka 39 hadithi hii sasa imetengenezwa filamu. Ni filamu nzuri iliyojaa ufundi wa hali ya juu wa upigaji picha na imechezwa na wahusika wanaojua sanaa ya filamu ni nini.
Nilipoonana na Mzee Hammie Rajab swali la kwanza nililomuuliza ni muda wa filamu hiyo. Niliuona ni muda mrefu kuiangalia. Hata yeye anasema mwanzoni ilikuwa dakika 150 wakaona ni ndefu mno, wakaipunguza zikabaki dakika 120, wakaona ni chache mno. Wakabaki wameduwaa na kuwaachia watazamaji waamue kama ni filamu ndefu au fupi. Kitu alichonihakikishia ni kuwa hakuna matukio yaliyorefushwa ili kuwachosha watazamaji. Kutokana na kazi zake za kuongoza filamu za kibuyu, Rama, Zawadi, Mama, Nawaachieni, Ngome ya Mwanamalundi na Siri, ilibidi nilikubaliana naye.

Kutoka kitabu hadi filamu

Hammie anasema wamiliki wa filamu hiyo walielekezwa kwake na Mzee Faraj Katalabula. “… Katalambula alinifahamisha kuwa kuna watu wamenunua haki miliki ya kutengeneza filamu kutoka kitabu chake, na yeye amewaelekeza kwangu hivyo wakija niongee nao ili nione kama naweza kuwaandikia skripti na kuwaongozea filamu hiyo, nilikubali..” alisema Hammie wakati nilipotaka kujua aliingiaje kwenye uongozaji wa filamu hiyo.

kweli alifuatwa na Doroth Kipeja wa Tripod media ili aifanye kazi hiyo. Hammie alifanya kazi ya kuandika Skripti ya filamu hiyo kwa mwezi mmoja, na anakiri kuwa ilikuwa ni kazi iliyokuwa na changamoto kubwa kwa sababu ilibidi amfiche “Agness” ambaye ndiye alikuwa akifanya mauaji katika filamu hiyo. Kazi hiyo ilikuwa ngumu zaidi kwani Agness alikuwa muhusika mkuu akiwa ndani ya familia ya Mzee Jacob (Mzee Upara). “Ilibidi nimfiche” anasema Hammie na kuongeza kuwa hicho ndicho kinachofanya filamu hiyo iwe tamu kama pilau na kachumbari.

Uandikaji wa skripti

Hammie anaongeza kuwa alikuwa na wakati mgumu wakati wa kuandika Skripti ya Simu ya Kifo kwa sababu kuu tatu. Kwanza watu wengi ambao sasa ni watu wazima na hata vijana wamekisoma kitabu hicho hivyo asingependa kuwaangusha. Pili, hakupenda kumuangusha mzee Katalambula ambaye wamefahamiana zaidi ya miaka 30 ambaye ndiye alimpigia debe kuwa angeifanya filamu hiyo isitoke nje ya mtiririko mzima wa visa na matukio na tatu, alitaka Watanzania wapata kitu chenye ubora na waache kufikria kuwa filamu za nje ndio bora zaidi.

Filamu ya simu ya kifo kama nilivyotanabahisha awali ni filamu ya kipelelezi inayotokana na kitabu cha simu ya kifo. Kila mara Inspekta Wingo alipopata simu ilikuwa ni simu ya kifo iliyomjulisha kuwa kuna mtu ameuawa. Bahati mbaya muuaji ndiye aliyekuwa akimpigia simu inspekta.

Hammie anasema kuwa tofauti na filamu nyingine alizowahi kuandika, hii ya Simu ya kifo ukisoma Skripti yake unaiona filamu ndani ya karatasi.

Wahusika katika filamu ya Simu ya Kifo

Filamu hii imesheheni wachezaji wenye ujuzi mkubwa katika uigizaji na taaluma yenyewe ya filamu. Yumo Tekla Mjata (mama Bishanga) ambaye katika filamu hii amecheza kama Mke wa Mzee Jaboc. Huyu licha ya kucheza filamu pia ni Mhariri wa siku nyingi wa filamu aliyepata kufanya kazi Kampuni ya Filamu Tanzania miaka ya 1970. Yumo Mzee Fundi Saidi (Mzee Upara) ambaye aliwahi kuigiza filamu hii akiwa kama Inspekta Wingo enzi hizo filamu hii ikitoka kwenye gazeti la picha la Filamu Tanzania.

Katika orodha hiyo yupo Riama mwanadada aliyecheza Sinema ya Fungu la Kukosa. Hammie anasema alipomuona tu Riama alimkubali moja kwa moja. Walipoongea nae pia na yeye hakusita, alikubali. Ilibidi wamsubiri kwanza hadi amalize matatizo ya familia yaliyokuwa yanamkabili ndipo uzalishaji wa filamu hiyo ukaanza. “..Nilikuwa na hamu ya kufanya naye kazi na yeye pia alikuwa na hamu ya kufanya kazi na mimi..” anaongeza Hammie na kusema kuwa potelea mbali… angeweza kumsubiri muigizaji huyo hata kama ni kwa miezi sita kwa sababu ni dada anayejua nini cha kufanya mbele ya Kamera.

Yupo pia Hashim Ramsey, ambaye aliyecheza kama Inspekta Wingo. Hammie anamsifu Hashim kwa kuhifadhi mistari yake ya wenzake. Anasema aliwapa skripti na alipowaita kwa ajili ya mazoezi (rehersal) Hashim alikuwa anajua nini anasema na nini wenzake watasema. Haiishii hapo anasema kuwa huyu ni professional kwa sababu hapotezi hata sekunde. Yumo pia Mrisho Mpoto anayecheza kama Fambo. Hammie anakiri kuwa wapo wasanii wasio na majina ambao pia wamecheza vizuri.

Upigaji picha na mandari

Filamu hii imepigwa mjini Tabora, inaanza kwa kuonyesha maeneo ambayo mtu yeyote anayeijua Tabora atakiri kuwa imeutangaza mji huo. Anatania na kusema baadhi ya watu kama Benard Mapalala wa Business Times, Nuru Shija wa Uhuru, Jamila Abdala wa Changamoto, Swedi Mwinyi wa RTD na Rehani wa Bima ya Afya, na Miguel Suleiman wa the Citizen au hata Ismail Aden Rage wakiiona lazima itawakumbusha kitu. Hakufafanua. Ili kuipa msisimko filamu hiyo Hammie anasema ilibidi watumie majengo ya Jeshi la polisi. Mungu bariki Jeshi hilo liliridhia na filamu inaanza kwa kuonyesha kituo kikuu cha Polisi Tabora na kulivuta jengo hilo hadi ndani ambamo Inspekta Wingo anaonekana kajaa tele lakini baada ya sekunde chache anaanza kukiona kiti kichungu baada ya kuanza kupokea simu za vifo vya kutatanisha.

Hammie anasema kuna baadhi ya sehemu za hadithi hiyo ilibidi atengeneze maelezo (dialogue) kama vile kule Nzega ambako ambako Inspekta Wingo aliwakama wacheza kamari ambako kwenye maelezo ya kitabu haielezi Inspekta Wingo jinsi alivyowakamata wacheza kamari wa kule. Kama kawaida ya Hammie, filamu zake nyingi zimepigwa na Sylone Malalo wa Real times studio.

Matukio ya kukumbuka?

Yapo matukio kadhaa nje ya filamu anayoyakumbuka. Moja ni pale walipoenda kituo kikuu cha polisi ambapo polisi hakuwakujua kuwa yule aliyevaa mavazi ya kipolisi hakuwa askari. Wakaanza kumpigia saluti pale kituoni. Tuliwaomba radhi na kuwaambia kuwa yule hakuwa Inspekta bali tulikuwa tunatengeneza filamu anaongeza Hammie.

Waigizaji wa Sinema hiyo wote wanashukuru ukarimu wa wenyeji wa Tabora na kusema kuwa walipata ushirikiano mkubwa.

Uzinduzi wa filamu?

Hammie anakwepa swali hilo na kusema ni Doroth Kipeja (Producer) wa filamu hiyo ndiyo anaweza kulisemea suala hilo kuwa filamu hiyo itazinduliwa lini, na kumalizia kwa kusema anatazamia itakuwa hivi karibuni. “…… Kitu ambacho nina uhakika ni kuwa nakala za filamu hiyo zitakuwa hazitoshi…..”

Basi na tusubiri na kuona, ukishaiona pengine tutakuwa na mambo ya kuizungumzia filamu yenyewe. Kila la kheri, Mzee Hammie na wote walioshiriki utengenezaji wa Simu ya Kifo.

00000000000000000000000000000

Hashim Kambi "Inspekta Wingo" wakati wa matayarisho ya filamu ya Simu ya Kifo

Hashim Kambi "Inspekta Wingo" wakati wa matayarisho ya filamu ya Simu ya Kifo

One Response to “Filamu ya Simu ya Kifo imeitangaza Tabora Ulimwenguni”

  1. Anonymous Says:

    bahati mbaya sana sijaiona hiyo filamu ya simu ya kifo, natamani sana maana nilisoma kitabu hicho nikiwa mdogo, kimepotea nina hamu nacho na nina hamu ya kuiona hiyo filamu inauzwa wapi ? nina hamu sana nayo hiyo picha ?


Leave a Reply (Please be decent) Acha ujumbe wako hapa (kuwa mstaarabu)

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Uyui

A website about Uyui, Tabora heritages and the Wanyamwezi

Shahermohd's Blog

Just another WordPress.com site

WordPress.com

WordPress.com is the best place for your personal blog or business site.

%d bloggers like this: