Mwaliko wa COSAFA ni kama mlango uliokuwa wazi, hapakuwa na haja ya kuuvunja.

Mwaliko wa COSAFA ni kama mlango uliokuwa wazi, hapakuwa na haja ya kuuvunja.

Waswahili wanao msemo wao unaosema kuwa, mlango ulio wazi huwa hauvunjwi. Hofu yangu ni kuwa, huenda sisi na TFF ndio tunaelekea huko na hii ndio hoja yangu ya leo.

TFF hivi karibuni imesema kuwa wameshindwa kuipeleka timu ya taifa katika michuano inayoandaliwa na Baraza la vyama vya mpira wa miguu kwa nchi zilizo kusini mwa Afrika (COSAFA). Wametoa sababu. TFF imesema kuwa michuano hiyo imekuja wakati tayari walikuwa wamepanga ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea na ikizingatia pia kuwa kuna michuano ya Chalenji itayofanyika Kenya mwezi Novemba 28, itakuwa vigumu kwa Stars kushiriki michuano mingine. Michuano hiyo inatajaria kuanza Oktoba 17 mwaka huu.

Inawezekana sababu hizo ziko sawa au haziko sawa lakini wametoa sababu za kwanini wameshindwa kuipeleka timu huko. Hoja yetu si kuzijadili sababu zilizotolewa lakini kwa stahili hii tunayokwenda nayo, ukilinganisha na mataifa mengine na tujiulize kama kweli tunayo mategemeo ya kujikwamua katika soka letu hili la chumbani na sebuleni?

Zamani, kule kwetu bushi ya ushirombo tulikuwa tunawinda jolwe. Sijui kama jina hilo ni la kiswahili. Kwa wale watu wa mjini jolwe ni aina ya ndege ambaye ni mtamu sana. Wakati ule tulikuwa tunawinda kwa kutumia manati. Alikuwepo rafiki yangu mmoja ambaye angeweza kulenga jolwe bila kuachia manati yake mpaka jolwe anaruka kwenye mti na kutokomea. Alikuwa anatumia muda mwingi kulenga bila kupiga. Ndivyo tunavyotaka kuwa katika soka letu?

Katika dunia ya leo ambayo watu wanacheza mechi za makombe matatu katika juma moja, sisi hatuna muda lakini tunataka tuwe kama wao. Tunataka ratiba isiyobana. Nchi na mataifa mbalimbali duniani wanajiandaa kwa michuano ya mpira kama vile wanakwenda vitani, sisi tunataka muda wa kujiandaa, wakati tunafahamu fika kuwa mchuano ya kualikwa ni sehemu ya maandalizi ya kesho. Nani amesema kujifunza kunakwisha?

Juzi, timu zetu kubwa mbili zimeukataa mwaliko wa Micho na St George yake. Sitaki kusema kuwa fundi asiye na ujuzi husingizia vyombo vyake na wala sitaki kufikiria hilo. Siri ya ndani aijuaye mwenye nyumba. Nina uhakika kuwa TFF na vilabu vilivyokataa mwaliko ni watu makini na wana nia njema. Hoja yangu ni kujifunza kutokana na hili lililotokea sasa na haja ya kutouvunja mlango uliokuwa wazi. Hivi? Hatukuwa na njia nyingine mbadala zaidi ya kuuvunja mwaliko uliokuwa wazi? Hebu tufikirie kidogo.

Kwa miaka mingi ukanda huu wa CECAFA umekuwa ndio unaovuta mkia katika soka barani Afrika. Pengine ndio majaaliwa yetu. Kuna wenzetu kama Zambia na Malawi ambao walikuwa wanachama wa CEFACA lakini baadaye wakajiengua na wengine wamekuwa wakishiriki kama waalikwa wa michuano hii wa msimu. Sisi pamoja na ushiriki wetu, hali yetu ni ile ile. Ama kweli chako ni chako.

Kuna wakati kama nakumbuka vizuri, timu ya taifa ya Malawi ilishawahi kwenda mpaka sudan, ikapigwa chini kwenye michuano hii, kisa eti ilichelewa. Soka letu katika ukanda huu, tusipoangalia tutabaki tunacheza wenyewe kwa wenyewe, kama kusoma darasa la watu uliowazidi uwezo. Hupati changamoto zaidi na usipokuwa mjanja katika hilo ujue khatari inakunyemelea.

Sitaki sisi tufike huko na Mungu apishe mbali suala hilo lisitukute. Ilishwahi kusemwa huko nyuma kuwa nchi hii ina watu takribani milioni 40 na wapo wachezaji katika mikoa mbalimbali ya nchi hii, meneja wa sasa wa Taifa stars Leonard Mukebezi Tasso ni mfano wa kuigwa. Lakini tumeingiwa na ugonjwa wa kujaza wachezaji wengi kutoka simba na Yanga sijui kwa sababu ya kuogopa gaharama au kitu gani! Leo hii lazima tushindwe kupeleka timu kwa sababu karibu timu zote kubwa zinazoshiriki ligi kuu zina wachezaji zaidi ya watatu katika timu ya Taifa. Katika hali kama hiyo ligi lazima isimame na hakuna aliye tayari.

Wakati mwingine, huwa kuna hoja pana zinanijia na kujiuliza kama kweli tunakwenda mbale katika soka letu au tunarudi nyuma. Hii ni soka nzima kwa ujumla ikiwemo utayari na kuthubutu. Nakumbuka miaka ya 1980-90, tulishawahi kuwa na victoria na Kakakuona na zote zilikuwa timu za taifa. Hata kama mazingira ya kuandaa muchuano wakati ule yalitulazimisha kuwa na timu hizo, lakini lilikuwa ni darasa tosha ambalo hakuna aliyelikumbuka tena! Hivyo ndivyo tulivyo, hatujifunzi kutokana na mazuri seuze tunayokosea!

Hoja yetu ya leo ni kuganga yajayo. Kama tunataka kukimbia, lazima tuwe na timu ambayo itakuwa na sura ya kitaifa na iliyo na wachezaji wa mikoa mbalimbali. Tumechoka na Yanga na Simba au timu za Dar. Madhara yake ndiyo haya. Huko mikoani kuna watu wanacheza mpira wa hali ya juu. Wapo. Wapo wengi tu tena wana nidhamu ya hali ya juu. Tatizo letu hatujipi muda wa kufikiri zaidi au hatuna muda huo. Maximo akibadili kikosi analaumiwa kama kaua mtu, lakini madhara yake ya muda mfupi na muda mrefu ndio haya. Hatulaumu mtu, tunalaumu mfumo.

Kuna watu wana hoja kuwa unaweza kuwa na timu ya taifa yenye hata wachezaji 80 halafu ukiwa na mualiko au mashindano unachagua kutoka kikosi hicho. Sisi hatusemi uwe na wachezaji wengi kama Brasil, ukiwa nao 30 huwezi kushindwa kupata 18 na ukaenda kwenda michuano bila kuathiri ligi yako ya ndani kwa sababu kila timu itakuwa imetoa lau mchezaji mmoja. Haja labda uwe huna uhakika kama timu yako itawakilisha vizuri au itafungwa. Kama hoja ndio hiyo, basi kujitoa sio hoja, hoja ni kuimarisha kikosi chako cha timu ya taifa hata kama kufanya hivyo ni kuwa na timu B. Kama niwakanyaga vidole mniwie radhi. Ni mtazamo tu wa hoja pana kutoka kwa mtu wa kuja. magangaferuzi@gmail.com

Ipo hoja nyingine ambayo watu wamekuwa wakiisema kwa muda mrefu. Kuwapa wachezaji uzoefu wa kimataifa. Sisi michezo yetu mingi ni ya hapa hapa, ni nadra sana timu yetu inatoka nje ya mipaka ya nchi. Kilio chetu siku zote kimekuwa ni kupata michuano ya kimataifa ya kujipima nguvu. Tutajuaje uimara wa ngome yetu kama hatujashambuliwa? COSAFA kwangu mimi Maganga ilikuwa ndio fursa ya kuipima timu yetu. Baada ya hapo tungeelekea kwenye chalenji yetu ya kila siku (business as usual).

Wanaofanikiwa wote duniani ni watu wanaothubutu nje ya mazoea ya kila siku. Hili pengine ndilo ambalo watendaji na wasimamizi wa michezo tungewaomba kulitekeleza kwa sababu wanalijua.

Hoja yetu nyingine katika kuganga yajayo, ni kuitikia wito. Ukiwa mtu wa udhuru sana, siku nyingine wanaweza kukuchoka. Ingekuwa ni mimi Maganga ningewaambia kuwa tunawaletea timu kali, lakini siyo ile waliyoizoea. Mbona Kenya walipelekewa timu ya Brazil ambayo sio waliyoitegemea. Huwezi kujua mbona wakati wa Kakakuona tulifanya maajabu?

Hoja yetu ya mwisho kwa siku ya leo ni utayari. Katika dunia ya leo ni lazima tuwe tayari kwa jambo lolote. Na kila kitu tukiangalie kwa kupima uzito na faida zake. Mimi kwa mtazamo wangu finyu naona kuuvunja mwaliko wa COSAFA ni kama kuuvunja mlango uliokuwa wazi.

leo ni siku ya wazee

Leo ni siku ya wazee duniani. Uzee ni tija na tunu na unapaswa kuenziwa. Ni muhimu kuangalia ni kwa jinsi gani siku hii inafikia malengo yaliyokusudiwa.

Uyui

A website about Uyui, Tabora heritages and the Wanyamwezi

Shahermohd's Blog

Just another WordPress.com site

WordPress.com

WordPress.com is the best place for your personal blog or business site.