Filamu: Baada ya miaka 200 Mzimu wa Waluguru wa Kolelo Watengenezewe filamu


Baada ya miaka 200 Mzimu wa Waluguru wa Kolelo Watengenezewe filamu

kolelo

Kolelo: Baada ya miaka 200, mzimu wa kiluguru wa karne ya 19  watengenezewa filamu ya kusisimua.

________________________________________________________________________________________________________

 Mzimu wa kolelo uliopo kwenye pango la mlima Kolelo umeichagua familia ya Kunambi kusika mikoba ili iweze kuwakomboa watu wa Lubasazi, Uluguru, Unguu, Duthumi, Vigolegole, kolelo, mvuha, Lukwangule na maeneo mengine kutokana na madhila,  kuwapa tiba ya maradhi  na kuwaongoza katika maombi pindi majanga mbalimbali yanapotokea. Komwe, mtoto wa Kunambi anasita kwenda mlimani kuchukua mkoba baada ya baba yake kufariki. Haikumsaidia. Alitumiwa mjumbe mlimbwende aitwaye Ndelawasi ili waende, aliposuasua mjumbe yule akabadilika ghafla na kuwa ajuza mwenye sura ya kutisha na Komwe hakuwa na namna nyingine pasi na kufunga safari ya kuelekea mlimani. Fuatana na mwandishi Maganga Feruz katika simulizi za filamu hii zinazosimuliwa na Shemeji wa Komwe, Mzee Juma wasiwasi katika Kolelo- filamu iliyotengenezwa na Irene Sanga, Sylone Malalo na Hammie Rajab.

­­­­­­­­­­­___________________________________________________________________________________________________________________

 Ukiiona kolelo utaipenda

Hata wale wavivu wa kuangalia, nina imani kuwa filamu hii itaisha kabla hawajachoka kuiangalia.  Ni filamu-simulizi fupi, pengine fupi zaidi kuliko zote ulizowahi kuzisikia, kuzijua  au hata kuziona. Ni muda wa kama dakika 38 tu hivi na ushee unakuwa umemaliza kuiangalia filamu yote!

Cha ajabu ni kwamba pamoja na ufupi huo, ukiiona, nina imani lazima utaipenda. Watengenezaji wake angalau wamejitahidi kuepuka mtego wa kuirefusha bila sababu, wakaifanya  isheheni matukio yote muhimu kwa ufupi lakini bila kuyaharakisha. Kwa lugha ya kiarabu filamu hii ingeweza kuitwa jumlat-lmufida, yaani Muhtasari unaojitosheleza.

Kolelo ni tofauti na filamu tulizozizoea

Filamu ya kolelo iko tofauti kidogo na filamu nyingi tulizozizoea. Humu kuna masimulizi ya karne ya 19 yanayoambatana na matukio mnasaba unayoyaona kwenye filamu yenyewe. Ni masilimuzi ya Mjomba anayemsimulia mpwaye kuhusu hisitoria ya wazazi wake, kuhusu chimbuko lao na hasa kuhusu mzimu wa Kolelo. Katika filamu hii  unapata simulizi inayoambatana na picha.

Simulizi za kolelo kwa Ujumla.

Kolelo, jina la Mzimu maarufu sana Morogoro. Asili yake ni jina la mwanamke Ajuza, Bibi aliyepewa karama na Mwenyezi Mungu ya kutibu na kutatua matatizo ya watu mbalimbali huko mlima Kolelo, kwenye pango ambapo mzimu wake ulifanya maajabu. Alipofariki, mzimu wake uliendelea kuwachagua watu wa kurithi mikoba. Kaburi la Bibi huyu lipo mpaka leo huko Lubasazi (Kolelo halisi). Ukilitaka waone walinzi wa Mlima Kolelo.

Zipo simulizi lukuki kuhusu miujiza ya Kolelo na mlima wenyewe, kubwa ni ile ya ufumbuzi wa matatizo ya Jamii. Ikitokea shida yeyote ya kijamii kama kukosekana kwa mvua, magonjwa, au hata shida binafsi mfano, kukosa mtoto kwa muda mrefu baada ya ndoa na kadhalika, watu wanakwenda katika mlima wa Kolelo na kufanya maombi (tambiko). Wakifika mlimani hapo  watalia, watoa machozi, watawaweka watoto wadogo na vikongwe mbele (hawa wanaaminika kuwa ni wasafi) na baadaye watachinja mnyama na kurudi. Kama ni shida ya mvua hawatafika nyumbani wakavu, watafika wamelowa chapachapa.

Ipo simulizi moja ya mapokeo isemayo kuwa, kulikuwa na  wanawake wawili ndugu walioenda kusenya kuni msituni, bila shaka karibu na mlima Kolelo. Mmoja akapotea, inasadikiwa alibebwa na joka hadi pangoni wakamtafutaaa… wakakata tamaa. Baada ya muda akatokea, akarudi akiwa na mkoba, mkoba wa Uganga! Ni mkoba huo aliorudi nao kutoka pango la Kolelo ndio alioutumia kuikomboa jamii dhidi ya madhila,  mkoba huu ukarithiwa kutoka kizazi hadi kizazi.

Ya Kolelo unaweza kusema ni ya zamani, lakini yapo ya sasa. Kama unaamini Mungu, basi jua kuwa kuna watu ambao Mungu amewapa karama. Juzi juzi tu hapa mlinzi mwingine wa milima ya Uluguru, Kingalu mwana Banzi wa 14 alisema haina haja ya Taifa kuingia gharama ya kutengeneza mvua na kwamba wao (kina Kingalu) bado wapo.

Kolelo ni mahala pasafi, wachafu hawafiki huko, ama sivyo wataumbuka. Sio uchafu wa mwili au mavazi, ni uchafu wa matendo na tabia. Ujumbe wa Kolelo ni kuwataka watu walirudie usafi wa matendo,  wazirudie mila na desturi. Kazi kweli kweli!

 Kolelo iliyotengenezewa filamu

Kama nilivyoeleza awali, zipo simulizi na matukio mengi yanayohusu Kolelo, Waluguru na mila zao zilizojaa urithi mwingi. Marehemu Mbaraka Mwinshehe Mwaruka aliwahi kuimba kuhusu Tambiko la Wahenga na wimbo mwingine wa Bondwa ugenda iii. Zipo simulizi za Kondoo wa Radi, na mambo ya milima ya unguu. Machache yamesemwa, mengi hayajasimuliwa wala kuandikwa. Urithi unapotea.

Filamu hii inatokana na kitabu cha Hammie Rajab, kiitwacho Miujiza ya Mlima Kolelo alichokiandika miaka ya 1980. Watengenezaji wa Kolelo wamechukua tukio moja tu,  la mtu na mkewe waliokaa muda wa muda takribani miaka mitano bila kubahatika kupata mtoto. Wenza hawa wakashauriwa. “kwanini hamuendi Kolelo? Wakaamua kufunga safari kwenda kolelo. “….. Unataka nikuambie kama walipata au hawakubahatika….? Mmh itafute Kolelo uone mwenyewe jinsi watoto wa mizimu wanavyokuwa au itafute filamu iitwayo Kibuyu.

Nilimuuliza mmoja wa Wakurugenzi wa filamu hii, Irene Sanga (mtunzi wa ule nyimbo ya salamu zangu kwako Mjomba) kwanini wameibana sana Kilelo kwa kuchagua tukio moja tu la mtu aliyetaka mtoto na wakaacha mengine kama ya mvua? Akanijibu kuwa wao wamechokoza tu! Watunzi wengine wanaweza kuibua Kolelo nyingine ikaogelea kitu kingine kwani matukio yapo mengi na kuyaeleza yoye kwenye filamu moja unaharibu ladha na kulipua kazi. Nilikubaliana na Irene Sanga, japo kwa shingo upande.

 Wahusika ndani ya filamu ya kolelo

Upo mseto wa majina makubwa na chipukuzi. Mzee Kunambi (Fundi Saidi/Mzee Kipara) yeye humu anayecheza kama mzee Kunambi. Huyu ni mkongwe katika fani. Yupo mama Thekla Mjata na Riama Ally (wanaocheza kama ndelawasi) wasanii wote hawa wamecheza pia filamu ya Simu ya Kifo iliyotengemezwa na Tripod Media ambayo nayo ni moto. Yupo Irene Sanga anayecheza kama mke wa Komwe (Issa Shamte), yumo Mrisho Mpoto na Issa Shamte (Komwe) anayecheza kama mtoto wa Mzee Kunambi anayetakiwa kurithi mikoba ya Kolelo. Ni wahusika wanaojua wanafanya nini. Hawapayuki kama wapo jukwaani.

Wamo pia wanakijiji wa Lubasazi, (lubasazi ndio Kolelo yenyewe)  ambao sina uhakika kama watabahatika kuiona filamu hii. Syllone Malalo ananitoa wasiwasi kuwa waliahidi kuirudisha Kolelo kwa wenyewe ili waione. Natamani iwe kesho!

 Upigaji wa picha,  na mandhari.

Picha za filamu hii zimepigwa na kuhariririwa na Syllone Malalo. Malalo ni mmoja wa watu anayeijua vilivyo kazi yake. Ni mbunifu. Katika Kolelo amejitahidi kuonyesha madhari halisi huku akibadili mikao ya kamera (camera angles)  kwa ustadi mkubwa. Ninathubutu kusema kuwa amefanikiwa kurudisha akili za watu kifikira kurudi vijijini walikotoka. Nyumba za udongo, taa za koroboi, hali ya kijani kibichi, uoto wa asili. Mavazi ya heshima. Lugha zisizo na mchanganyiko kwa kiswa-kingereza na mengineyo mengi.

Hadhari kubwa imechukuliwa kulinda uasili wa Kolelo ambayo, asili yake ni masimulizi yaliyorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi kutokea karne ya 19 au hata nyuma yake. Upigaji picha wake pia unafuata mkondo huo huo. Upigaji picha wa aina hii hutumika kuelezea au kuonyesha matukio ya zamani za kale. Kwa ufupi Kolelo ni filamu-jarida au kama ni lazima kusema Kiingereza ndio ieleweke basi hii ni Documentary-film au kwa ufupi ina muundo wa Docu-film.

 Midundo na mirindimo inayosisimua.

Katika Kolelo kumepigwa sana mbeta, mbeta la kiluguru ambalo sasa hivi ukilitaka labda ufungulie RTD (tumbizo asilia), Radio Uhuru (karibu wataanza) TVT (ngoma zetu) au Radio Tumaini (chimbachimba muziki asilia na Che-Mundugwao) vinginevyo endelea na nyimbo za kimagharibi. Ipo siku nao watapiga nyimbo zetu!?

Wanaopenda ngoma asilia hasa zumari la mbeta, kwenye Koleo hapo watakuwa wamepata ile kitu roho inapenda. Mirindimo ya  ngoma hiyo pamoja na muziki uliotungwa na Irene na Msangi wenye mahadhi ya Reggae ya asili, roots ndivyo vinavyofanya mseto wa midundo murua ya zamani hadi siku hizi.

Nilimuuliza Irene kisa cha kuweka Reggae wakati filamu inaanza akaniambia kuwa wakati mwingine inabidi uchanganye na usasa kidogo uwavute watu wa rika zote hasa vijana wa leo.  Kwa hili sikukubaliana naye.

 Mila na tamaduni za kale

Katika mambo ambayo kina Irene  wanayojaribu kuyarudisha katika jamii ni ile mila ya kujizuia kufanya ngono hasa kwa mgeni ambaye hujamfahamu. Wanasisitiza ukarimu na msaada kwa mtu mwenye shida bila kumdai chochote kama malipo. Marehemu Hemed Maneti wa Vijana Jazz alishawahi kuimba kuhusu Chiapo, kuwa akimtendea  wema mtoto wa kike asijaribu kudai ujira wa mapenzi, a-jali asante.

Katika sehemu ya filamu hii tunamuona msichana, binti mzuri wa haja aitwaye Ndelawasi (Riyama Ally) kutoka Lukwangule, anapiga hodi kwa Komwe akiomba hifadhi. Anaomba msaada apelekwe Kolelo. Anakaa wiki nzima akila na kunywa bila kuombwa penzi.  Wote damu zinachemka lakini hakuna chuchuchu.

Kuna sehemu kolelo inatisha na kusisimua

Nani kasema wafu huwa wanarudi tena kuishi duniani? Nani ataamini kuwa kikongwe aliyofariki miaka kadhaa iliyopita tena akiwa na zaidi ya miaka 80 anaweza kujigeuza akaja kama binti mrembo wa miaka 18? Mbele ya macho yako? Si utachanganyikiwa? Uone binti anabadilika kuwa kikongwe halafu wakati huo huo anarudi kuwa msichana? Usikie ngurumo!!! Uone mlima unatikisika!! Haya ni baadhi tu ya matukio yaliyo ndani ya filamu hii. Utaogopa?

Yapo pia matukio ya  kuku kutoweka mikononi mwa aliyemshika na mtu kusikia sauti ambayo mwenza wake waliye jirani hasikii kitu kabisa.

Matukio ya kukumbuka nje ya filamu

Irene anasema safari ya kuelekea Kolelo kiasi inaogofya, kule hakuna mawasiliano ya mawimbi yeyote ya simu. Mungu bariki walisafiri salama kwenda na kurudi bila kuharibikiwa. Huku akionyesha kushukuru Mungu, anasema sijui ingekuwaje kama wangeharibikiwa kwa sababu hata magari kule yanapita kwa msimu.

Nilipomuuliza kuhusu mandhari ya Kolelo akasema alifurahia mambo mengi kikiwemo chakula cha kitoweo cha kuku wa kienyeji na sana alifurahia kuoga mtoni. Akaongeza kuwa kule wanaume wanaoga sehemu yao na wanawake wanaoga sehemu yao. Akakumbuka simulizi za moto mkubwa ambao uliishia kuuzunguka mlima miaka miwili iliyopita bila kuunguza hata jani la mlima. Akaongeza kuwa kuna wazungu walitaka kuingia mlimani bila kuomba ruhusa kwa walinzi wa mlima. Mpaka leo hawajulikani walikopotelea.

Kilio cha Irene Sanga

Kolelo ni zao la jitihada za Irene Sanga kutaka urithi wa Kolelo usipotee. Nilipata kumueleza Hammie Rajab kuwa Irene Sanga ni m-mila, akatasamu asinijibu kitu. Sikushangaa na wala yeye hakushangaa. Niliuliza swali ambalo jibu lake tayari nilikuwa nalo mkononi. Katika vita hii ya kuipigania urithi wetu, wapo makamanda ingawa sina uhakika na jeshi. Baadhi ya watanzania wapo, wapo watanzania mahiri kwelikweli  wanaojitahidi kudumisha mila na utamaduni kupitia sanaa katika mazungumzo yao, mavazi na fikra zao. Wapo wanakerwa na utamaduni wa kimagharibi.

 Kizazi cha luninga

Ipo hoja kwamba Sasa tupo katika Ulimwengu wa utandawazi huwezi kuishi kama kisiwa. Mimi sipingani na hoja hii. Swali ambalo najiuliza ni kuwa, huu utandawazi upo kwetu tu? Mbona Bara Hindi, Korea Kusini, Italia na kwingineko bado wanadumisha mila, utamaduni na urithi wao?

Najua ni vigumu, pengine ni ndoto ya mchana kurudia maisha ya uzamani. Marehemu Shaaban Robert alishawahi kuongelea ukale na usasa miaka kadhaa iliyopita. Kwa kuwa tumeziachia luninga ndio ziwalee watoto wetu pengine sisi hatuna muda wa kuwasilimulia wanetu hekaya na simulizi za mashujaa wetu kama mama Deborah Mwenda wa TVT na mama na mwana ya zamani RTD, basi angalau tuwanunulie  watoto na familia zetu kanda na filamu zinazoelezea asili na utaifa wetu.

 Kaditama

Nawahimiza watunzi na waja asili kama kina Merinyo wa Afrika sana, Benard Mapalala (kwa heri Iselamagazi), Ben Mtobwa na Mbogo (Ngome ya Mwanamalundi), Sisi Tambala, Mzee Jangala, Saidi wa Ngamba (mzee small), Farham Mohammed na Gumbo Kihorota (Itunyama) waendelee. Siwezi kuwataja wote orodha ni ndefu, lakini shime endeleeni. Potelea mbali, hata kama si leo iko siku vizazi vijavyo vitakuja kutanabahi na kuithamini asili, chimbuko na urithi wetu. Faraja ninayoipata ni kuwa angalau watakuwa na pa kuanzia kupitia filamu, wimbo, mavazi na simulizi zenu. Maasalamu.

https://uyui.files.wordpress.com/2013/05/kufungia-stori-1.jpg?w=1042&h=47

Advertisements

One Response to “Filamu: Baada ya miaka 200 Mzimu wa Waluguru wa Kolelo Watengenezewe filamu”

  1. John Valentine Says:

    Safi Sana


Leave a Reply (Please be decent) Acha ujumbe wako hapa (kuwa mstaarabu)

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Uyui

A website about Uyui, Tabora heritages and the Wanyamwezi

Shahermohd's Blog

Just another WordPress.com site

WordPress.com

WordPress.com is the best place for your personal blog or business site.

%d bloggers like this: